Thursday, March 15, 2012

TIBA MBADALA YA MAGONJWA SUGU

Kama inavyofahamika katika jamii yetu kuna watu wengi ambao wamekumbwa na magonjwa yanayotajwa kuwa hayana tiba na wengine wapo njiani kuambukizwa maradhi ya aina hiyo.

Inakuwaje pale unapokwenda hospitali na kukutana na jibu la dokta likikufahamisha kuwa wewe ni muathirika wa Ukimwi au unakabiliwa na kansa au kisukari.

Utawaza nini ukisikia mumeo ana uvimbe kwenye ini?. Utamjibu nini rafiki yako atakapokutaka umshauri kuhusu uvimbe wa hatari uliogundulika katika ubongo wake?

Bila shaka maneno na mawazo lazima yatatofautiana sana. Kwa anayeumwa kauli ya kujipa moyo kuwa atapona inaweza kutoka kinywani lakini mawazo yakabaki na jawabu la kifo kwa asilimia 80 au pengine hata zaidi ya hapo. Hivyo basi, kipimo cha kufa katika mawazo kitakuwa juu ya kile cha kupona.

Kwa maana hiyo, mawazo ya kufa yanaposhinda maradufu zaidi ya ya yale ya kupona, yanazalisha nguvu za kutimiza kile ambacho mwili unapewa taarifa kutoka katika ubongo ambao ndiyo muongozo na chaji ya vitendo vyote vinavyofanywa na viungo vya mwili wa mwanadamu.

Kanuni ya kisaikolojia inayosema kuupa mwili hisia za kifo ni sawa na kupanda umauti ambao mhusika atake asitake atavuna kifo.

Kinachotajwa hapa ni kwamba, kutafuta tiba ya ugonjwa wa kansa ambao mwanadamu ameshaamini kwa mawazo kuwa hauponyeki na kifo ndiyo suluhisho ni kuhangaika bure kumeza dawa ambazo kimsingi hazitafanya kazi inayokusudiwa na matabibu.

Labda kabla haujazama ndani ya mada hii naomba niseme wazi kuwa mimi sina lengo la kupinga watu wasiende hospitali, isipokuwa nataka jamii yenye magonjwa sugu ifahamu tatizo la kwanza kutibiwa si

kansa, Ukimwi, kisukari, pumu na BP, bali tiba ya kwanza lazima ihusishe namna akili inavyoweza kutafsiri magonjwa hayo.

Kabla mgonjwa hajaamua kwenda hospitalini au kumeza vidonge, anatakiwa kuyaondoa mawazo yake kutoka kwenye mfereji wa kifo hadi kwenye matumani ya kuishi licha ya kuambukizwa Ukimwi.

Akishafanya hivyo na kutoshtushwa na hofu ya kufa, atakuwa anaufanya mwili wake kuimarisha kinga zaidi ya kupambana na ugonjwa wake hata kabla ya kuanza kutumia madawa.

Katika utafiti wa hivi karibuni ulioripotiwa katika jarida la New England la Marekani umethibitisha kuwa, watu wenye hofu na kukata tamaa wana hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa kwa uwiano wa 2-1 ukilinganisha na watu ambao wanaishi kwa imani.

Pia utafiti mwingine uliofanyika hivi karibuni nchini Marekani uliowahusisha panya waliofungiwa chombo cha kuwafanya wakate tamaa na wengine kuachwa katika hali yao ya kawaida na baadaye kupandikizwa saratani, waliofungiwa chombo cha hofu walibainika kuambukizwa mara mbili zaidi ya wale ambao hawakuwa na hofu.

Ukweli uko hivi, kinachochangia vifo vya watu wengi sio magonjwa yenyewe bali ni hali za wagonjwa kukata tamaa, jambo ambalo husababisha kinga za mwili kumeng’enywa kwa kiwango kikubwa na kumfanya mgonjwa adhoofike haraka na kuzifanya dawa anazomeza kushindwa kufanya kazi katika kiwango kilichokusudiwa na hatimaye mgonjwa kupoteza maisha yake.

Kutokukata tamaa ni tiba ya kwanza na yenye nguvu zaidi ambayo inaweza kumfanya mgonjwa aishi hata kama amepata maambukizi ya magonjwa ya hatari. Nasema hivi kwa sababu mwenendo wa dunia una nguvu asili ambayo hushughulika kuwaondoa watu waliokata tamaa na kuwaacha watu imara wenye kuamini katika kuishi kwao.

Kwa maana hiyo ili mwenye ugonjwa usiokuwa na tiba aishi muda mrefu lazima kwanza aondokane na hali ya kukata tamaa.

Ni suala la lazima kufuta uongo wa kimawazo kwamba Ukimwi, kansa kisukari ni magonjwa ya kifo, ingekuwa ndivyo watu wasingekufa kwa ajali, badala yake wangesubiri wapate kansa ndiyo wafe. Kifo hakina ubia na magonjwa hayo kwani hata wazima wanakufa.

Jambo jingine kubwa kabisa ambalo watu wengi hawalifahamu ni kuhusu watu wanaotakiwa kuwa karibu na mgonjwa. Imebainika kuwa mara nyingi wagonjwa huwa hawajifahamu hali zao pale wanapokuwa wanaumwa. Kwa maana hiyo majibu ya hali zao huyapata kutoka kwa watu wanaowauguza au wale wanaofika kuwatazama.

Mgonjwa anapotazamana na rafiki yake aliyepo kitandani kwake na akakutana na maneno ya kusikitikia hali yake kutoka kwa wanaomtazama, kwa mfano: “Oooh pole sana ndugu yangu yaani umekwisha kwa muda mfupi hivi, ama kweli ugonjwa wa TB si wa kuchezea” tayari kwa maneno hayo mgonjwa aliyeko kitandani ambaye hafahamu madhara ya ugonjwa wake huingiwa na hofu.

Tangu hapo ataanza kuhisi kuwa ni mtu aliyekonda sana, hisia ambazo zitazidi kumuongoza katika mawazo ya kujiona yu karibu na mlango wa kuzimu. Kwa mantiki hiyo watu wanaowaguza au kuwajulia hali wagonjwa wanatakiwa kuwa na maneno yenye faraja hata pale hali ya mgonjwa inapoonekana kuwa ni ya kukatisha tamaa.

Mgonjwa anatakiwa kuwekwa mbali na mazungumzo yanayoelezea ukubwa wa maradhi yake na jinsi watu wanavyokufa kutokana na ugonjwa wa aina yake. Maneno ya kumkejeri na pengine kumbagua kimaisha ni mambo yanayotakiwa kuepukwa na wauguzaji.

Lengo la kufanya hivi ni kumtibu mgonjwa kiakili na kumfanya ajione ni wa kupona, licha ya kuugua kwa muda mrefu.

Pamoja na hayo inashauriwa kwamba watazama wagonjwa na wahudumu wawe na maneno yenye mzaha utakaofanya mgonjwa awe na fursa ya kucheka au kutabasamu kwa furaha. Hii itamsaidia mgonjwa kupunguza kiwango cha sumu inayozalishwa mwilini mwake.

Ni vizuri pia watu wakafahamu kuwa mazoezi kwa wagonjwa na lishe ni vitu muhimu sana kuliko hata vidonge. Ni vema wagonjwa wakapewa mazoezi kulingana na ushauri wa matabibu na muda mwingi wafarijiwe kwa kupewa vitabu, kutazama video, kusoma majarida na katuni za kuwapotezea mawazo ya kuugua kwao. Kwa wale ambao hawana nguvu wanaweza kubembelezwa kwa maneno ya faraja.

Hayo yote yakifanyika mgonjwa atakuwa na nafasi ya kupona na kuishi kwa muda mrefu hata kama atakuwa na maradhi sugu yasiyokuwa na tiba. Watu wanaokwenda makanisani kuombewa (kwa mfano) hawapewi dawa ila wanatiwa imani ya kwamba watapona.

Tiba ya faraja imekuwa ikitumika zaidi nchini Marekani na Uingereza na imeonesha mafanikio makubwa. Hospitari nyingi hasa wa watoto zimekuwa zikifungwa televisheni zinazoonesha michezo ya kuchekesha eneo la mapokezi na madaktari wamekiri kuwa watoto hupata nafuu hata kabla ya kuingia kwenye chumba cha Daktari.

Ushauri wa mwisho kwa wagonjwa wote wenye magonjwa sugu ni kuacha woga wa kufa badala yake wayapokee matatizo yao na kuyashughulikia kwa imani kuwa yanawezekana kutatuliwa. Ulimwenguni kuna watu wengi ambao wameishi miaka mingi wakiwa na UKIMWI, KANSA, KISUKARI, MOYO na mpaka leo hawana dalili za kufa.

Kinachowaua wengi kama nilivyosema ni hofu si magonjwa husika. Uchunguzi unaonyeha kuwa hata wanaodhurika mapema na virusi vya ukimwi ni wale waliopokea majibu yako na kukata tamaa ya kuishi.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment